Thursday, February 9, 2017

SHAMBA LA MITI KAWETIRE

Shamba la Miti Kawetire  lipo katika Wilaya ya Mbeya Vijijini Mkoani Mbeya, ndani ya msitu wa hifadhi ya Usafwa kaskazini na Safu ya mlima Mbeya. Shamba lipo kilimita 12 kutoka Mbeya mjini katika barabara kuu ya Mbeya – Chunya.

Shamba lilianzishwa mwaka 1937 na serikali ya kikoloni kwa madhumuni ya uzalishaji wa kuni kwa ajili ya migodi ya dhahabu  ya Chunya.

Ili kutimiza azma hiyo miti jamii ya mikaratusi ilipandwa katika eneo la Ipinda. Upanuzi ulifanyika mwaka 1942, 1950 na 1974 kwa kupanda miti jamii  ya misindano (Pinus spp) na mikambokambo (Cupressus lusitanica) na kulifanya shamba lililopandwa kufikia ukubwa kama ilivyo sasa.

Baada ya uhuru madhumuni ya mashamba ya miti likiwemo la Kawetire yaliboreshwa kwenda sambamba na Sera  ya misitu ambayo ni;
  • Kuhakikisha upatikanaji endelevu wa mazao na huduma za misitu kwa kuwa na maeneo ya kutosha na yenye usimamizi madhubuti.
  • Kupanua ajira na kuongeza pato la fedha kutokana na maendeleo endelevu katika viwanda vinavyojikita kwenye misitu.
  • Kuimarisha mifumo ikolojia kwa kuhifadhi bioanuwai ya misitu maeneo ya lindimaji na rutuba ya udongo.
  • Kukuza uwezo wa taifa katika kusimamia na kuendeleza sekta ya misitu kwa kushirikiana na washikadau wengine.
Eneo la Shamba la Miti Kawetire lina msimu mmoja wa mvua ambapo huanza kunyesha mwezi Novemba na kuendelea hadi mwezi  April mwaka unaofuata

Mtiririko unaonesha kwamba miezi ya Juni na Oktoba ni mikavu na kati ya Juni na Agosti ni kipindi cha baridi kali na mara nyingine hali ya joto hufikia nyuzi -5  ̊C hasa wakati wa usiku.

 Kwenye miezi ya joto ya Oktoba na Novemba kiasi cha joto hufikia nyuzi joto 35  ̊C.

Shamba la miti kawetire lina ukubwa wa  hecta 5,280 ambazo zimegawanyika kama ifuatavyo ;

Eneo lililopandwa miti limeongezeka kutoka hekta 1,563 mwaka 2012/2013 hadi hekta 2,720 mwaka 2015/2016 hii inamaanisha upandaji umefanywa katika maeneo mapya kwa ukubwa wa hekta 1,157 kuanzia mwaka 2012/2013 hadi 2015/2016.
Maelezo ya maeneo
Hekta
Eneo lililopandwa miti (mpaka 2012)
1,563
Eneo la upanuzi lililopandwa miti 2012/2013 – 2015/2016
1,157
Jumla la eneo lilipandwa miti
2,720
Eneo la upanuzi ambao halijapandwa miti(makadirio)
471
Jumla kuu
3,191
Eneo la msitu wa asili ni hekta 1,572 na eneo hili limejumuisha maeneo yenye vyanzo vya maji.

Kwa ajili ya usimamizi shamba limegawanywa katika sehemu sita zinazojulikana kama Safu. Shamba hili linaongozwa na Meneja wa shamba ambaye anawajibika kwa Mtendaji Mkuu Wakala wa Huduma za Misistu Tanzania (TFS).Meneja wa Shamba ana meneja msaidizi. Safu husimamiwa na wakuu wa safu.Hawa pamoja na wakuu wa vitengo mbalimbali kama vile Uvunaji na leseni, Miundombinu, Ulinzi wa msitu na Nyuki,Uhasibu na Ugavi huwajibika kwa meneja wa Shamba.

Shamba lina watumishi wa kudumu 34 wa kada mbalimbali na watumishi wa mkataba 9, Maafisa misitu (4), Wasaidizi Misitu wa Stashahada na Astashahada (7), Wasaidizi Misitu (20), Mhasibu (1), Katibu Muhtasi (1) na Tabibu (1).Aidha kutokana na ufinyu wa watumishi tuna watumishi wanaofanya kazi kwa mkataba wa mwaka mmoja mmoja ambao ni madereva (2), Walinzi (6), Fundi bomba (1).

Shamba lina mpango wa Usimamizi (Management Plan) wa kipindi cha miaka mitano.Mpango huo wa usimamizi ndio mwongozo wa kuendesha Shamba na kuandaa mipango kazi na bajeti za kila mwaka (Annual Plan of Operations). Mpango wa usimamizi wa sasa ulianza 2012/2013 hadi 2017/2018.
Mpango huu unahusisha kazi zifuatazo
  • ·       Kazi za shambani (Ukuzaji wa miche ya miti katika bustani iliyopo Kawetire na Mbeya Peak) kuandaa mashamba kwa ajili ya upandaji miti katika maeneo yaliyovunwa na katika maeneo ya upanuzi (Extension area), Upandaji miti,usafi wa mashamba (sanitary slashing), kupogoa matawi, doria kwa ajili ya ulinzi wa msitu,ujenzi na ukarabati wa barabara za msituni na uvunaji miti.
  • Kazi za utawala na mafunzo (Mikutano, Mafunzo ya muda mfupi, safari za kikazi, likizo za watumishi, ujenzi na ukarabati wa majengo na nyumba za kuishi watumishi, uendeshaji wa magari,manunuzi mbalimbali na kazi za utawala kwa ujumla)
Katika mwaka wa fedha 2012/2013 Jumla ya hekta 275 zilipandwa kwenye maeneo ya upanuzi na hekta 95 kwenye maeneo yaliyovunwa miti.Hii inafanya jumla ya eneo lililopandwa kwa mwaka huo kuwa hekta 370.

Katika mwaka wa fedha 2013/2014 Jumla ya hekta 165 zilipandwa katika maeneo ya upanuzi katika Safu ya Lwanjiro na Ipinda na hekta 129 zilipandwa katika maeneo yaliyovunwa katika safu za Kawetire na Ipinda.

Kwa kipindi cha miaka mitatu ya fedha tumekuwa tukivuka lengo la upandaji kwani katika mwaka wa fedha 2012/2013 upandaji ulikuwa 149%. Kwa mwaka wa fedha 2013/2014 upandaji ulikuwa 156.5% na 2014/2015 upandaji ulikuwa 112% haya ni mafanikio makubwa kwa shamba na Wakala kwa ujumla.

Changamoto iliyopo ni kuhakikisha kwamba nguvu na gharama kubwa iliyotumika kwa ajili ya upandaji miti haipotei.Tumeweka mikakati ya kuhakikisha miti inatunzwa kwa uangalizi wa hali ya juu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha tunafanya usimamizi wa karibu ili kuilinda miti.

Shamba la miti kawetire tumekuwa tukikusanya maduhuri ya serikali yanayotokana na uuzaji wa miti ambapo   mwenendo wa ukusanyaji  maduhuri ni kama ifuatavyo. 
FY
Volume
TOTAL
2012/13
        6,867
       344,968,053
2013/14
      17,636
       823,327,314
2014/15
      17,737
       882,335,080
2015/16
      12,168
       498,150,755
TOTAL
      54,408
   2,548,781,202

Katika shamba la miti Kawetire tumeanzisha mradi wa ufugaji nyuki na hadi sasa tuna mizinga ipatayo 100 kati ya hiyo mizinga  yenye nyuki kwa sasa ni 31.
   
Katika taarifa za miaka iliyopita moja kati ya changamoto ambazo zimekuwa zikionekana kwenye taarifa hizo ni uchakavu wa nyumba za watumishi, na baadhi ya nyumba hizo zilijengwa mwaka 1937, kimsingi nyumba ni chakavu na nyingi zinahitaji kubomolewa kwani hazifai tena kufanyiwa ukarabati.Kwa nyumba ambazo zina unafuu wa kufanyia ukarabati, tumefanikiwa kufanya ukarabati mkubwa na mdogo pamoja na ujenzi wa vyoo. Ukarabati huu unaendelea kufanyika kadri bajeti inavyoruhusu. Hii ni katika kuhakikisha kwamba watumishi wanaishi katika mazingira ya kuridhisha na masafi.

Pamoja na shughuli za upandaji miti na shughuli mbalimbali shamba linawezesha na kutoa huduma mbalimbali kwa jamii inayozunguka shamba na taifa kwa ujumla.Uwezeshaji na huduma hizi ni kama ifuatavyo;

Shamba linaajiri vibarua wa kutwa zaidi ya 600 kwa mwaka kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za shamba, vibarua wengi huajiriwa wakati wa upandaji miti, kutengeneza barabara za moto na ulinzi wa misitu; wengi wa vibarua ni wenyeji wa mbeya kutoka vijiji vinavyozunguka shamba.

Wafanyakazi wa shamba na wanavijiji hugawiwa maeneo ya kulima katika maeneo yaliyovunwa miti. Wastani wa watu 300 hufaidika na huduma hiyo ambayo utaratibu huu hutoa mchango kwenye usalama wa chakula (food security) na kuongezea wananchi mapato.

Wananchi waishio jirani na shamba huruhusiwa kuokota kuni kavu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Wananchi wanaruhusiwa pia kutafuta mboga katika maneo ya msitu.

Shamba la Miti Kawetire linatoa mchango katika huduma za afya na maendeleo ya wananchi kwa ujumla. Kuna zahanati moja ambayo hutoa huduma ya matibabu kwa wanavijiji na watumishi wa shamba. Zahanati hii imekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha huduma za afya za watumishi na wanavijiji wa jirani zinaimarika kwa kutoa elimu juu ya lishe bora na elimu ya kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi (VVU).

Shamba pia linachangia katika sekta ya ujenzi kutokana  na mauzo ya miti ambayo inachanwa mbao zinazotumika kwenye ujenzi.

Katika kuunga mkono agizo la Mh. Raisi wa Jamhuri ya Mungao wa Tanzania kwamba lazima kila mtoto akalie dawati Shamba la Miti Kawetire limeanza kutengeneza madawati 264 ambayo yatagawanywa katika Shule mbalimbali za Wilaya ya Mbeya.

Changamoto mbalimbali zinazolikabili shamba ambazo ni pamoja na:-
Kusitishwa kwa upandaji wa eneo la upanuzi safu ya Karuwe
Eneo hili lilikuwa ndani hifadhi yam situ wa safu ya mlima mbeya lenye ukubwa wa hekta 1280. Eneo hili likuwa  linavamiwa na wananchi mara kwa mara  na kufanywa eneo la malisho, kilimo na uwindaji hivyo kupelekea matumizi ya moto wakati wakiendesha shughuli zao na kusababisha mioto ya mara kwa mara na hivyo kuharibu uoto uliokuwepo.

Kutokana na sababu hiyo eneo hilo lilihamishwa kutoka kwenye usimamizi wa Kanda na kuhamishiwa kwa Shamba la Miti Kawetire kwa ajili ya kupanda miti ili kurudishia uoto uliokuwepo, hii ilikuwa ni pamoja na kupanda miti ya kibiashara na kuhakikisha kwamba Sheria ya mazingira inafuatwa kwa kuacha vyanzo vya maji umbali wa mita 60 au zaidi.

Upandaji huu ulizingatia kwamba, maeneo yaliyo mbali na vyanzo vya maji yapandwe miti ya kibiashara na yale yaliyo karibu na vyanzo vya maji yapandwe miti rafiki ifaayo maeneo hayo ikiwamo na utunzaji vyanzo hivyo.

Upandaji ulianza Januari 2016 na baada ya kupanda hekta 295 kati ya 478 zilizotakiwa kupandwa 2015/2016, tulipata zuio kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwamba tusiendelea kupanda wala kuhudumia miti iliyokwishapandwa kwani kulikuwa na malalamiko kutoka Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira ya jiji la Mbeya kwamba tunaharibu vyanzo vya maji.

Shamba la miti kawetire hupata matukio ya moto ambao kwa kiasi kikubwa husababishwa na shughuli zinazofanywa na wananchi wanaozunguka msitu kama vile uwindaji, uandaaji wa mashamba na kurina asali. Matukio haya hupunguza jitihada za usimamizi endelevu wa shamba.

Katika kukabiliana na changamoto hii uongozi wa shamba la miti kawetire umekuwa ukifanya yafuatayo;
Kuelimisha jamii 
  • Vijiji kumi na sita vinavyozunguka Shamba hupewa elimu ya kuzuia na kupambana na moto kwa njia ya mikutano ya kampeni ya kudhibiti moto
  • Kikosi maalumu cha kupambana na moto  kinachofanya kazi saa 24 kwa siku kwa kipindi chote cha kiangazi
  • Kutengeneza barabara za kinga dhidi ya moto kuzunguka shamba lote kila mwaka
  • Kuchoma barabara za moto wakati ambapo nyasi hazijakauka sana ili kupunguza kasi ya moto pale unapotokea.
  • Kuweka ratiba kwa watumishi wote wa shamba kuwa tayari kupambana na moto pale unapotokea.
Shamba halina lori wala “tractor” kwa ajili ya kusaidia shughuli za bustani na upandaji jambo ambalo linafanya usafirishaji wa miche kwenda maeneo ya upandaji kuwa mgumu na kuchukua muda mrefu kwani wakati mwingine tunalazimika kutumia “L/c hardtop”
Ili kukabiliana na changamoto hii, katika mwaka wa fedha 2015/2016 shamba lilitenga bajeti kwa ajili ya kununua grader na tractor na mchakato wa manunuzi unaendelea na unafanyika na TFS HQ

Shamba lina upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali hasa madereva na walinzi.
Ili kukabiliana na changamoto hii shamba huajiri vibarua kwa mkataba wakati tukisubiri ajira za kudumu kutoka Serikalini.

Majengo na nyumba za watumishi zimechakaa kwani nyingi zimejengwa mwaka 1937.Nyumba nyingine hazifai hata kufanyiwa ukarabati kwani zimeanza kubomoka na kuta kuanza kudondoka.

Katika kukabiliana na changamoto hii pamoja na ufinyu wa bajeti Shamba limeweza kufanya ukarabati mkubwa wa majengo mawili ,nyumba ishirini na mbili za watumishi, ujenzi wa vyoo, majiko na ujenzi wa nyumba mbili za watumishi hii imepelekea kubadilisha muonekano wa mandhari ya nyumba na ofisi.
Eneo la msitu wa nishati wa mbeya (Mbeya fuel wood) lililokuwa na zaidi ya hekta 300 limekuwa likivamiwa na kupimwa viwanja na mpaka sasa eneo lililobaki ni kama hekta 67 tu.

Katika kukabiliana na changamoto hii na kulinusuru eneo lilobaki uongozi wa Shamba umelipima eneo kwa kushirikiana na Ofisi ya Kanda ya Nyanda za juu Kusini na Halmashauri ya jiji la Mbeya katika kuandaa mpango kabambe ili kuinua utalii wa Mikoa ya Nyanda za juu Kusini. Kazi hii inaendelea na ipo katika hatua ya upimaji na upangaji wa viwanja kwa ajili ya makazi, mahoteli, nyumba za ibada, viwanja vya michezo na maeneo yatakayo hifadhiwa.
Share:

0 comments:

Post a Comment

International Day of Forests 2017

Search This Blog

Powered by Blogger.