Tuesday, February 21, 2017

TANZANIA, MSUMBIJI YAKUBALIANA KUTHIBITI UVUNAJI NA USAFIRISHAJI HARAMU WA MAZAO YA MISITU KATIKA MIPAKA YA NCHI HIZO

Kaimu Mtendaji Mkuu Wakala wa Huduma za Misitu nchini, Dos Santos Silayo (mwenye suti nyeusi) akijadiliana jambo na watendaji wa TFS na Mkurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori na Mazingira Duniani(WWF) Msumbiji, Bi. Anabela Rodriques (mwenye miwani) kabla ya kuanza kwa zoezi la kusaini hati ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Msumbiji, jijini Maputo jana kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu hususan mbao katika mipaka ya nchi hizo mbili. Wengine ni Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi ya Rasilimali wa Wakala wa Misitu nchini Bw. Mohamed Kilongo (mwenye suti) na mwakilishi wa WWF Tanzania, Bw. Geofrey Mwanjelwa.

Kaimu Mtendaji Mkuu Wakala wa Huduma za Misitu nchini, Dos Santos Silayo (mwenye suti nyeusi) akisaini kusaini hati ya makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Msumbiji, jijini Maputo jana kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu hususan mbao katika mipaka ya nchi hizo mbili. Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Mazingira na Maendeleo Vijijini, Bi. Sheila Afonso pamoja na mtendaji wa Wizara hiyo (hakuweza kufahamika jina lake mara moja).



Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu nchini imefanya mazungumzo na kusaini hati ya makubaliano na Serikali ya Msumbiji kupitia Wizara ya Ardhi Mazingira na Maendeleo Vijijini mjini Maputo Msumbiji jana kuthibiti uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu katika maeneo mipaka ya nchi hizi mbili.

Akisaini makubaliano hayo yaliyoratibiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori na Mazingira Duniani(WWF)kupitia mradi wa Crossboaders, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu, Prof. Dos Santos Silayo alisema makubaliano hayo yatasaidia kukabiliana na changamoto za udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu hususan mbao katika mipaka ya nchi hizo mbili.

“Makubaliano haya kati ya Tanzania na Msumbiji yatasaidia kupiga vita biashara haramu ya mbao pamoja na mazao ya misitu inayofanyika kupitia mipaka ya nchi hizi, biashara ya uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa za misitu baina ya nchi hizi umekuwa na tija kutokana na kukua kwa soko la nyumba. Hivyo kwa pamoja tukishirikiana tutaweza kuhakikisha sheria, taratibu na kanuni za uzalishaji na usafirishaji wa mazao ya misitu zinafuatwa,” alisema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Mazingira na Maendeleo Vijijini, Sheila Afonso alipongeza hatua hiyo muhimu iliyofikiwa na kuahidi kuwa Tanzania itaendelea kuwa rafiki na ndugu wa dhati wa Msumbiji kama ambavyo mahusiano ya nchi hizi mbili yamejengwa tangu zamani.
Share:

0 comments:

Post a Comment

International Day of Forests 2017

Search This Blog

Powered by Blogger.